BALOZI DK. ASHA-ROSE MIGIRO AFIKISHA SALAMU ZA RAIS DKT. SAMIA KWA WANANCHI WA KINONDONI NA UBUNGO
09 Jan, 2026
37 Machapisho
Ubungo / Kinondoni – Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, amewasilisha salamu za pongezi na shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa wananchi na wanachama wa CCM wa Wilaya za Ubungo na Kinondoni.
Akizungumza na wanachama wa chama wa CCM na maelfu ya wananchi, Balozi Dkt. Migiro amesema Rais Samia anatoa pongezi za dhati kwa kazi kubwa inayofanywa na wanachama katika kuimarisha chama, hususan katika ngazi za chini kuanzia Mashina, Matawi hadi Kata, ambazo ndizo mhimili mkuu wa uhai na ushindi wa CCM.
“Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapongeza sana kwa namna mlivyojitoa kwa hali na mali wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi, kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinapata ushindi mnono,” amesema Balozi Dkt. Migiro.
Ameeleza kuwa mafanikio ya CCM yanatokana na kazi ya msingi inayofanywa na wanachama walioko karibu zaidi na wananchi, akisisitiza kuwa ngazi za Mashina, Matawi na Kata ndizo zenye jukumu kubwa la kuimarisha mshikamano wa chama, kuhamasisha ushiriki wa wananchi na kulinda misingi ya demokrasia ya nchi.
“Ni kwenye ngazi yenu ndugu zangu Mashina, Matawi na Kata ndipo kazi kubwa imefanyika. Hapa ndipo wanachama na wananchi walipo, na hapa ndipo chama kinapopata nguvu yake ya kweli,” ameongeza.
Balozi Dkt. Migiro pia amewahimiza wanachama kuendelea kuwa macho, hai na wenye mshikamano, huku wakiheshimu misingi ya demokrasia inayoruhusu vyama na wadau mbalimbali kushiriki katika mchakato wa kuunda serikali, kwa lengo la kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya taifa.
Kwa kumalizia, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuijenga CCM kuanzia ngazi za chini kama mkakati endelevu wa kuhakikisha chama kinaendelea kuwa imara, chenye kukubalika kwa wananchi na chenye uwezo wa kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa ufanisi.
#ShinaLakoLinakuita
Habari Zinazohusiana
KATIBU MKUU WA UVCCM KUONGOZA KIKAO CHA SEKRETARIETI YA BARAZA KUU LA UVCCM, ZANZIBAR
09 Feb, 2026
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Ndugu Halid Mwinyi (MNEC), anatarajiwa kuongoza kikao cha Sekretarieti ya Baraza Kuu la UVCCM kitakachofanyika Jumanne, tarehe 10 Februari 2026, katika Chuo cha Umoja wa Vijana Tunguu, Zanzibar.
RAIS DKT. SAMIA AZINDUA SOKO JIPYA LA KARIAKOO: AFUNGUA UKURASA MPYA WA TUMAINI LA KIUCHUMI, AAGIZA HAKI, UWAZI NA USALAMA KWA WAFANYABIASHARA
08 Feb, 2026
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amezindua rasmi Jengo Jipya la Soko la Kariakoo
RAIS DKT. SAMIA AAGIZA UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU, UJENZI WA KITUO CHA WATOTO NA ELIMU YA ZIMAMOTO SOKO JIPYA LA KARIAKOO
08 Feb, 2026
Dar es Salaam 08 Februari 2026 Katika kulinda uwekezaji wa umma na kuhakikisha thamani ya fedha za wananchi inalindwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kutunza na kusimamia miundombinu ya Soko