UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

RAIS DKT. SAMIA AZINDUA SOKO JIPYA LA KARIAKOO: AFUNGUA UKURASA MPYA WA TUMAINI LA KIUCHUMI, AAGIZA HAKI, UWAZI NA USALAMA KWA WAFANYABIASHARA

08 Feb, 2026 13 Machapisho
Dar es Salaam
08 Februari 2026
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amezindua rasmi Jengo Jipya la Soko la Kariakoo, tukio lililoashiria kufunguliwa kwa ukurasa mpya wa matumaini ya kiuchumi na uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kulinda ajira, kurejesha kipato na kuimarisha hadhi ya biashara za Watanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Dkt. Samia amesema ujenzi wa Soko Jipya la Kariakoo ni nguzo kubwa ya shughuli za kiuchumi kwa maelfu ya Watanzania wanaotegemea biashara kama chanzo kikuu cha maisha yao.
“Tunapozindua Soko Jipya la Kariakoo leo hii, tunafungua ukurasa mpya wa tumaini na nguzo kubwa ya shughuli za kiuchumi kwa Watanzania wengi wanaotegemea biashara,” amesema Rais.
Rais ameeleza kuwa soko hilo ni sehemu muhimu ya mfumo wa biashara wa taifa, likiwa ni kitovu kinachowaunganisha wazalishaji wa mazao ya kilimo na viwandani, wasafirishaji, wauzaji na wanunuzi, si tu kutoka ndani ya Tanzania bali pia kutoka nchi jirani.
“Soko hili ni sehemu muhimu kibiashara kwa nchi yetu, linaunganisha mzalishaji wa mazao ya kilimo au ya viwandani, msafirishaji, muuzaji pamoja na mnunuzi,” amesisitiza.
Katika kueleza dhamira ya Serikali, Rais Samia amesema uamuzi wa kujenga upya Soko la Kariakoo ulilenga kurejesha kipato cha wafanyabiashara, kulinda ajira zilizokuwepo na kuimarisha hadhi ya biashara ya ndani, akibainisha kuwa huo ndio uhalisia wa falsafa ya Kazi na Utu.
“Serikali imechukua jitihada za kulijenga upya soko hili la Kariakoo kwa lengo la kurejesha kipato, kulinda ajira na kuimarisha hadhi ya biashara ndani ya nchi yetu, na huu ndio uhalisia wa kazi na utu,” amesema.
Katika msisitizo wa uongozi bora na haki za kiuchumi, Rais Dkt. Samia ameelekeza kuwa upangaji wa maeneo ya kufanyia biashara ndani ya soko hilo jipya lazima uzingatie haki, uwazi na usawa, bila upendeleo wa aina yoyote.
Amesema hatarajii kusikia wafanyabiashara wakipata maeneo kwa misingi ya ukaribu na viongozi, urafiki au ushawishi usio halali, na kulitaka Shirika la Masoko Kariakoo kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu.
“Sipendi kusikia kwamba kuna wafanyabiashara wamepata maeneo kwa upendeleo. Shirika la Masoko Kariakoo lifanye kazi yake ipasavyo,” amesisitiza Rais.