UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

RAIS DKT. SAMIA AAGIZA UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU, UJENZI WA KITUO CHA WATOTO NA ELIMU YA ZIMAMOTO SOKO JIPYA LA KARIAKOO

08 Feb, 2026 13 Machapisho
Dar es Salaam
08 Februari 2026
Katika kulinda uwekezaji wa umma na kuhakikisha thamani ya fedha za wananchi inalindwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kutunza na kusimamia miundombinu ya Soko Jipya la Kariakoo kwa nidhamu na uwajibikaji wa hali ya juu.
Rais amesema jengo hilo limejengwa kwa fedha za Watanzania, hivyo ni wajibu wa uongozi wa soko na wafanyabiashara kulitunza, kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuepuka vitendo vya uzembe au uharibifu vinavyoweza kulikosesha taifa faida ya uwekezaji huo mkubwa wa kimkakati.
Katika hatua nyingine inayogusa ustawi wa kijamii na utu wa wafanyabiashara, Rais Dkt. Samia ameuagiza uongozi wa Soko la Kariakoo kutenga eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kulea watoto kwa ajili ya akina mama wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao sokoni hapo.
Amesema uwepo wa kituo hicho utasaidia kuwaondolea akina mama mzigo wa kuunganisha malezi ya watoto na uendeshaji wa biashara kwa wakati mmoja, hali itakayoongeza ufanisi, tija na utulivu wa kisaikolojia katika mazingira ya kazi.
“Sasa ninyi mtatoa eneo, lakini akitokea mtu binafsi atakayekuwa tayari kuweka kitengo hicho cha kulea watoto pamoja na vifaa vyake, mumkaribishe,” amesema Rais.
Kupitia agizo hilo, Rais Samia amewaalika wadau wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa huduma za kijamii ndani ya soko, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi wa wafanyabiashara, hasa wanawake.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Samia ameliagiza Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kutoa mafunzo maalum ya kukabiliana na majanga ya moto kwa wafanyabiashara wote watakaofanya shughuli zao katika jengo hilo jipya. Amesema elimu ya tahadhari, matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto na uelewa wa taratibu za dharura ni msingi muhimu wa kulinda maisha, mali na biashara.
Hatua hiyo inalenga kupunguza madhara na kasi ya hatari zinazoweza kujitokeza, hususan ikizingatiwa historia ya majanga ya moto katika masoko makubwa ya mijini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, Soko Jipya la Kariakoo linahudumia takribani watu 200,000 kila siku, huku wafanyabiashara 1,520 wakithibitishwa kufanya shughuli zao ndani ya jengo hilo lenye gorofa sita na miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya biashara za ndani na za kikanda.
Soko hilo pia ni kitovu muhimu cha biashara ya mipakani, likihudumia wafanyabiashara na wanunuzi kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati, zikiwemo Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi, jambo linalolifanya kuwa soko la kimkakati katika uchumi wa kikanda.
Kwa ujumla, maagizo haya ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanaendelea kuakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi jumuishi, salama na unaojali utu wa wafanyabiashara, huku miundombinu ya biashara ikitambuliwa kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya taifa.