Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)
KATIBU UVCCM TABORA MJINI AANZA RASMI ZIARA YA KITENDAJI KATA ZA IKOMWA NA KAKOLA | UVCCM
Habari Nyingine

KATIBU UVCCM TABORA MJINI AANZA RASMI ZIARA YA KITENDAJI KATA ZA IKOMWA NA KAKOLA

26 Mar, 2026 Admin User 22 views min read
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Tabora Mjini, Cde. Muzamir Kambuga, tarehe 25 Machi 2026 ameanza rasmi ziara ya kitendaji katika Kata za Ikomwa na Kakola, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhai wa Jumuiya na kuongeza ufanisi wa shughuli za vijana.
Ziara hiyo inalenga kuhuisha na kukagua uhai wa UVCCM katika ngazi za kata na matawi, kusikiliza na kutatua changamoto za vijana, pamoja na kuhamasisha uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi ya Jumuiya. Aidha, Katibu Kambuga amesisitiza umuhimu wa usajili wa wanachama wapya kupitia mfumo rasmi, pamoja na kuhimiza utekelezaji wa vikao vya kikanuni kwa kuzingatia kalenda ya chama na Jumuiya zake.
Katika ziara hiyo, ameelekeza pia namna bora ya uandaaji na uandishi wa mihutasari ya vikao, kuhamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, na kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri kwa ajili ya vijana. Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa kila kaya kujiunga na bima ya afya, hususan mpango wa shilingi 150,000 kwa watu sita, ili kuboresha ustawi wa afya ya jamii.
Katibu Kambuga ameambatana na Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Wilaya ya Tabora Mjini, Cde. Juma Tandala, katika kuhakikisha ziara hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na inaleta matokeo chanya kwa vijana na Jumuiya kwa ujumla.
Taarifa hii imetolewa na Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Wilaya ya Tabora Mjini.