Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)
CHADEMA YAFANYA VIKAO VYA SIRI KUHAMASISHA VURUGU KUPITIA MAANDAMANO, CCM INATAKA WANANCHI KUDUMISHA AMANI | UVCCM
Habari za Kitaifa (UVCCM) Kipaumbele

CHADEMA YAFANYA VIKAO VYA SIRI KUHAMASISHA VURUGU KUPITIA MAANDAMANO, CCM INATAKA WANANCHI KUDUMISHA AMANI

13 Jun, 2026 Admin User 25 views min read

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Kenani Laban Kihongosi, amesema CCM imepokea taarifa inazodai ni za kuaminika kuwa viongozi wa CHADEMA wamefanya vikao vya siri vinavyolenga kuhamasisha maandamano na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kihongosi amesema CCM inatoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa walinzi wa amani, umoja na mshikamano wa Taifa kwa kutokubali kushawishiwa kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Amesema maendeleo endelevu yanategemea mazingira ya amani na utulivu, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji na ujenzi wa uchumi wa Taifa.

"Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama, yenye amani na utulivu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," amesema Kihongosi.

CCM YARIDHISHWA NA KASI YA MAENDELEO

Katika hatua nyingine, Kihongosi amesema CCM imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ameeleza kuwa mafanikio yanayoonekana katika sekta za afya, elimu, maji, umeme, miundombinu na uwezeshaji wa wananchi ni matokeo ya utekelezaji madhubuti wa sera na mipango ya Serikali.

Aidha, amesisitiza kuwa amani, umoja na mshikamano ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa, huku akionya dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi na kuathiri safari ya maendeleo ya wananchi.