Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)
KATIBU MKUU UVCCM MWINYI, CCM NI TANURI LA KUPIKA VIONGOZI, KIMBILIO LA VIJANA WENYE NDOTO ZA UONGOZI TOFAUTI NA VYAMA VYENYE MLENGO WA SACCOS | UVCCM
Habari za Kitaifa (UVCCM) Kipaumbele

KATIBU MKUU UVCCM MWINYI, CCM NI TANURI LA KUPIKA VIONGOZI, KIMBILIO LA VIJANA WENYE NDOTO ZA UONGOZI TOFAUTI NA VYAMA VYENYE MLENGO WA SACCOS

21 Jun, 2026 Admin User 14 views min read

Katibu Mkuu wa UVCCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Halid Mwinyi, amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (Chama Cha Mapinduzi) kinaendelea kuwa taasisi ya kimkakati kwa malezi, mafunzo na uandaaji wa vijana wenye ndoto za uongozi, akikitaja kama “tanuri la kupika viongozi” na kimbilio sahihi la vijana wasomi nchini Tanzania.

Akizungumza leo Juni 21, 2026, akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Mwanza yaliyofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu (BoT), Mwinyi alieleza kuwa mfumo wa CCM umejengwa katika misingi ya kuibua, kuwajenga na kuwapa nafasi vijana kushiriki moja kwa moja katika uongozi kuanzia ngazi za chini hadi kitaifa.

Alibainisha kuwa mabadiliko ya uongozi ndani ya CCM ni sehemu ya utamaduni wa kidemokrasia unaolenga kuimarisha taasisi badala ya watu binafsi, akisisitiza kuwa hilo ndilo msingi wa uimara wa chama hicho kwa muda mrefu.

“Kubadilishana uongozi ni utamaduni wa kawaida ndani ya CCM na ni sehemu ya demokrasia yetu inayojenga taasisi imara,” alinukuliwa akisema Mwinyi.

Aidha, alieleza kuwa CCM imekuwa ikiwekeza katika ujenzi wa uongozi wa vijana kupitia jumuiya zake na mifumo ya ndani inayowaandaa wanachama kuanzia ngazi za elimu ya juu hadi uongozi wa kitaifa, ambapo wengi wao hatimaye huingia katika nafasi mbalimbali za utumishi wa umma na chama.

“Chama chetu ni tanuri la viongozi tangu vyuoni mpaka ngazi za juu. Ushahidi upo kuna vijana wengi wamepikwa, wameiva na sasa wanakitumikia chama na taifa katika nafasi mbalimbali,” alisisitiza.

Katika hotuba yake, Mwinyi aliikosoa mitazamo ya baadhi ya vyama vya siasa, akidai kuwa havina mifumo madhubuti ya kuendeleza uongozi wa vijana na badala yake vinajikita katika ajenda zisizo na tija kwa maendeleo ya kitaasisi ya vijana.

Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutazama zaidi taasisi zenye mifumo thabiti ya mafunzo na fursa za uongozi, akieleza kuwa ndoto za uongozi zinahitaji mazingira ya sera, mafunzo na ushiriki wa moja kwa moja katika maamuzi.

Tukio hilo la mahafali limewakutanisha mamia ya wasomi na wanachuo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, likijadili nafasi ya vijana katika uongozi na maendeleo ya taifa.

#KazinaUtuTunasongaMbele

#NeverAgain