UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU AAGIZA MKANDARASI KUKAMATWA NA KUZUIWA KUSAFIRI

21 Nov, 2025 60 Machapisho
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameliagiza Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji kumkamata na kuzuia hati ya kusafiria ya mkandarasi anayejenga mradi wa Kituo cha Ukaguzi cha Pamoja (One Stop Inspection Station) kilichopo Muhalala, mkoani Singida.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali ilimwamini mkandarasi huyo na kumpa jukumu la kutekeleza mradi huo muhimu wa kimkakati, ambao umesimama kwa zaidi ya miaka nane tangu mwaka 2016. Mradi huo, unaotekelezwa na kampuni Impresa di Costruzioni Ing. E. Mantovani S.p.A, ulipaswa kukamilika mwaka 2018 lakini umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu.

Ametoa agizo hilo leo, Ijumaa 21 Novemba 2025, wakati akikagua mradi huo katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida, ziara ambayo pia inahusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.

Amesema licha ya jitihada kubwa za Serikali kuhakikisha mradi unasonga mbele, mkandarasi amekuwa akiweka ugumu katika utekelezaji wake. “Mkandarasi huyu alitangazwa kuwa amefilisika na hawezi kuendelea na mradi. Alipewa maagizo ya kulipa fidia kwa Tanzania kwa sababu amechelewesha utekelezaji,” amesema Dkt. Mwigulu.

Akiendelea kusisitiza, Waziri Mkuu ameagiza hatua kali zichukuliwe mara moja:
“Naelekeza Kamishna wa Uhamiaji akamate hati yake ya kusafiria. Asitoke nje ya nchi hadi jambo hili liishe. Hii ni hujuma ya waziwazi; ni dharau kubwa kwa nchi yetu. Jeshi la Polisi mtafuteni mkandarasi huyu popote alipo. Tumemuajiri, tunamlipa, lakini anajiamulia kama aendelee na kazi au la—huyu ni mhalifu. Akamatwe mpaka suala hili likamilike,” amesisitiza.

Dkt. Mwigulu ameonya kuwa wakandarasi wa nje wanapaswa kuelewa kuwa wanapokuja kufanya kazi nchini, wanatekeleza majukumu chini ya taratibu za Tanzania, na siyo vinginevyo. “Wasijione kama wao ni mabosi. Tanzania ndiyo imewaajiri,” amesema.

Aidha, ameelekeza washirika wa mradi huo kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanatoa kauli ya mwisho kuhusu kuendelea au kutokuendelea na mradi huo. “Wakishindwa kuendelea, Waziri wa Ujenzi uwapatie wakandarasi wadogo wamalizie kazi. Hii nchi ni yetu, na tuna wajibu wa kuilinda. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametuambia—hatuna mjomba, tuna mama mmoja tu anaitwa Tanzania,” amesisitiza.