UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

KAMBIRO: AMANI NDIO MSINGI MAENDELEO YA TAIFA LETU

05 Dec, 2025 54 Machapisho

Kigoma Mjini, 5 Desemba 2025

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini, Ndugu Comrade Haruna Kambiro, leo ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda na kuthamini amani kama nguzo kuu ya ustawi na maendeleo ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 5 Desemba 2025, Kambiro amesema kuwa amani na uhuru ndivyo vinavyoipa Tanzania uwezo wa kuendelea mbele kiuchumi, kijamii na kisiasa. Amesema licha ya Serikali kutokuwa na dini, Watanzania wana imani zao binafsi, hivyo viongozi wa dini wana jukumu kubwa la “kujenga imani, kutuliza jamii na kuimarisha umoja.”

Akiwashukuru waandishi wa habari kwa kazi ya uzalendo wanayoifanya kila siku katika kulinda amani kwa kutoa taarifa sahihi, Kambiro amesema CCM Kigoma Mjini inampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hotuba yake ya hivi karibuni aliyoitoa kwenye kikao cha Baraza la Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kambiro, hotuba hiyo ya Rais Samia “imetupa dira ya mbele, imekemea kwa uthabiti vitendo vyote vya uvunjifu wa amani, na imesisitiza umuhimu wa kufuata njia za kikatiba na kidemokrasia katika kudai haki.”

Akirejea matukio ya 29 Oktoba 2025, Kambiro amesema kuwa njia zilizotumika na baadhi ya watu—ikiwemo vurugu, uchomaji wa mali na uharibifu wa miundombinu—hazikuwa sahihi na haziwezi kuhalalishwa kwa sababu yoyote. “Amani haiwezi kujengwa kwa moto, vurugu au hasira. Amani ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote,” amesema.

Ameongeza kuwa Wanaccm Kigoma Mjini wanaungana kikamilifu na msimamo wa Rais Dkt. Samia katika kulinda utulivu wa nchi, na kwamba tofauti za vyama, imani au mitazamo hazipaswi kutugawa kama taifa.

Kambiro aliendelea kwa kusema:
“Niwaombe sana Watanzania wenzangu, hasa vijana bila kujali tofauti zetu au itikadi zetu tutangulize maslahi ya Taifa mbele. Amani ni jukumu letu sote. Sisi wanakigoma mjini tunabaki imara katika kuilinda na kuitetea.”

Taarifa hii imesisitiza dhamira ya CCM Kigoma Mjini kuhakikisha misingi ya amani, umoja na maendeleo inaendelea kudumu nchini, ikiwa ni mwendelezo wa kujenga taifa lenye mshikamano na dira thabiti ya ustawi wa kijamii.