UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

RAIS MWINYI AISHUKURU SERIKALI YA OMAN KWA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA ZANZIBAR

10 Oct, 2025 6 Machapisho

Zanzibar, 09 Oktoba 2025

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Oman na kupongeza uhusiano mwema wa kindugu na kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Oman.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo  tarehe 09, Oktoba 2025, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Kale na Utalii wa Oman, Mheshimiwa Sheikh Salim bin Mohammed Al Mahrouqi, aliyefuatana na Balozi Mdogo wa Oman anayefanya kazi zake Zanzibar, Mheshimiwa Said Salim Al Sinawi, pamoja na ujumbe kutoka Wizara hiyo ya Oman.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza dhamira ya Serikali ya Zanzibar kuendeleza uhusiano huo wa kihistoria kwa manufaa ya pande zote mbili, hususan katika maeneo ya utalii, utamaduni na uhifadhi wa urithi wa kihistoria.

Kwa upande wake, Waziri Mahrouqi amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa ukarimu wake na kueleza dhamira ya Serikali ya Oman kuendeleza ushirikiano uliopo, hususan katika programu ya ukarabati wa majengo ya kihistoria yanayofadhiliwa na Oman.

Akiwa Zanzibar, Waziri Mahrouqi, akiwa na mwenyeji wake Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mheshimiwa Mudrick Ramadhan Soraga, ametembelea majengo mbalimbali yanayofadhiliwa na Serikali ya Oman, yakiwemo Beit al Ajaib, Mtoni Palace, Kibweni Palace pamoja na majengo mengine yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.