SERIKALI IMETOA TRILIONI 3.5 KUWAWEZESHA VIJANA – MAJALIWA
10 Oct, 2025
11 Machapisho
Mbeya, Oktoba 10, 2025
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kutoa zaidi ya shilingi trilioni 3.5 kufikia mwaka 2024 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi, ikilinganishwa na shilingi bilioni 904 zilizotolewa mwaka 2021.
Amesema fedha hizo zimewasaidia vijana wengi kupata mitaji iliyowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, hivyo kuinua vipato vyao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Ijumaa Oktoba 10, 2025, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yaliyofanyika jijini Mbeya, yakibeba kaulimbiu isemayo: “Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu.”
> “Serikali imechukua hatua hizi kwa kutambua kuwa vijana ni nguvu kazi ya Taifa na ndiyo msingi wa safari ya maendeleo ya nchi yetu. Vijana wakipewa nafasi na kuandaliwa ipasavyo, wanaweza kuwa nguzo kuu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs),” alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa vijana wamekuwa nguzo muhimu ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, biashara, teknolojia, michezo na sanaa.
> “Katika nyanja za ubunifu na teknolojia, vijana ndiyo vinara wa matumizi ya teknolojia mpya na majukwaa ya kidijitali, ikiwemo akili mnemba (artificial intelligence) na mifumo ya mawasiliano ya kisasa. Michango yao imekuwa kichocheo cha mabadiliko chanya katika jamii na uchumi wa Taifa,” aliongeza.
Vilevile, Mhe. Majaliwa alitoa wito kwa wadau wote kuhakikisha vijana wanashirikishwa kikamilifu katika ngazi zote za maamuzi sio kama wanufaika wa sera pekee, bali pia kama wabunifu na viongozi wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Akiwa ametembelea banda la VETA, Waziri Mkuu alitoa wito kwa taasisi hiyo pamoja na wadau wengine wa elimu kuwapa kipaumbele vijana wenye ulemavu, kwa kuwapatia mafunzo maalumu na nyenzo muhimu za kujifunzia ili waweze kutumia ujuzi wao kujiongezea kipato.
> “Baada ya kutembelea banda hili, nimejifunza kwamba wapo vijana wenye ulemavu walio na vipaji na ujuzi mkubwa. Wazazi tuwe tayari kuwapeleka watoto wetu wenye ulemavu katika taasisi za elimu ili wapewe nafasi ya kujifunza na kujiendeleza,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb), alisema Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kundi la vijana na ndiyo maana inaendelea kuwekeza kikamilifu katika kukuza uwezo wao.
> “Hii ni rasilimali kubwa ambayo ikielekezwa ipasavyo na kujengewa uwezo kupitia vipaji walivyonavyo italeta maendeleo endelevu, kujenga taifa shindani na lenye ustawi,” alisema Ridhiwani.
Habari Zinazohusiana
KURA YANGU SAUTI YANGU
26 Oct, 2025
Ni haki yangu kushiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025
KAWAIDA: "WATAKE WASITAKE CCM ITASHINDA KWA KISHINDO KIKUBWA TAREHE 29"
26 Oct, 2025
Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa komredi Mohammed Ali Kawaida akizungumza na wananchi walio jitokeza kwa wingi katika Ufungaji wa Kampeni Jimbo la Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
MARTINE AHAMASISHA WAPIGA KURA KUBEBA KADI ZAO OKTOBA 29 NA KUTIKI KWA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN
26 Oct, 2025
Dar es Salaam, Oktoba 25, 2025 Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa wa Vyuo na Vyuo Vikuu Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Ndg. Emanuel Martine, amewahamasisha wafanyabiashara, wajasiriamali, wateja na wadau mbalimbali wa Soko la Mabibo jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba 2025, wakichagua kwa kishindo wagombea wote wa CCM.